yanga

Kumrithi Nchunga Yanga 200,000/-


Katibu Mkuu wa Yanga, Selestine Mwesigwa



Somoe Ng`itu

Fomu ya kuwania nafasi ya mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa klabu ya Yanga katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Julai 15 itatolewa kwa ada ya Sh. 200,000 imeelezwa jana.

Yanga itafanya uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi hizo mbili na nane za Wajumbe wa Kamati ya Utendaji kutokana na waliokuwa wanashikilia nafasi hizo kujiuzulu wakati mjumbe, Theonest Rutashoborwa, alifariki dunia.

Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu Mkuu wa Yanga, Selestine Mwesigwa, alisema kuwa zoezi hilo litaanza kufanyika Juni mosi kama maelekezo kutoka katika Kamati ya Uchaguzi ya TFF yalivyosema huku akiongeza kwamba taratibu nyingine zitatangazwa wakati wowote kuanzia leo.

"Tayari sekretarieti imeshaanza mchakato huo ila maelekezo mengine yatatangazwa na Kamati ya Uchaguzi ya Yanga baada ya kufanya nao kikao," alisema Mwesigwa ambaye ndiye anaiongoza Yanga kwa sasa kwa mujibu wa katiba yao.

Alisema pia fomu za nafasi ya Ujumbe wa Kamati ya Utendaji zitatolewa kwa gharama ya Sh. 100,000 na amewataka wanachama ambao si hai kuhakikisha wanalipia kadi ili wasipoteze haki yao ya kuchagua viongozi wanaowataka.

Aliongeza kuwa licha ya kusimamia zoezi la uchaguzi, vile vile wataendelea na zoezi la usajili wa wachezaji na maandalizi ya Kombe la Kagame ambapo Yanga ndio mabingwa watetezi.

Habari kutoka Yanga zinasema kuwa mkataba wa Mwesigwa umemalizika na hakukuwa na kikao sahihi cha Kamati ya Utendaji cha kumuongezea katibu huyo mkataba mpya.

Mwesigwa alisema kuwa mkataba wake ni siri na hivyo si sahihi yeye kuweka wazi kwa sababu ni makubaliano ya pande mbili.

Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Nchini (TFF) ilitoa maelekezo ya kuitaka Yanga ifanye uchaguzi baada ya wajumbe wake waliobakia madarakani kuwa wanne hivyo hawawezi kukutana na kutoa maamuzi yoyote kama katiba yao inavyoeleza.

Wajumbe ambao walibakia madarakani ni Salim Rupia, Sarah Ramadhani, Toto Ossoro na Mohammed Bhinda.

Viongozi waliojiuzulu ni pamoja na Mwenyekiti, Lloyd Nchunga, Davis Mosha (makamu), na wajumbe ni Seif Ahmed, Pascal Kihanga, Charles Mungodo, Ally Mayai na Mzee Yusuph.

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.