simba

Sakati la Yondani: Simba kumuwekea pingamizi


NA SOMOE NG`ITU

Beki mpya wa kati wa Yanga, Kelvin Yondani yuko hatarini kuikosa michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) baada ya klabu yake ya zamani, ‘Wekundu wa Msimbazi, Simba kutangaza kuwa itamuwekea pingamizi ili azuiwe kuwatumikia ‘Wanajangwani’ katika michuano hiyo itakayofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Jumamosi.

Uongozi wa Simba umesema jana kuwa Yondani bado ni mchezaji wao halali kwani Desemba 23 mwaka uliopita alisaini mkataba mwingine wa mwaka mmoja wa kuendelea kuichezea timu yao na kwamba watampinga kwa waendeshaji wa michuano ya Kagame, Shirikisho la Soka la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

Hivi karibuni, Yondani ambaye pia ni beki tegemeo wa timu ya taifa, Taifa Stars, alitambulishwa kwa mbwembwe mbele ya mashabiki wa ‘Wanajangwani’ na kuanza kujifua na klabu yake ya sasa kwa ajili ya michuano ya Kagame na pia msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wakiwa chini ya kocha mpya, Mbelgiji Tom Saintfiet.

Akizungumza na gazeti hili jana, Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu', alisema wanaamini kuwa Yondani ni mchezaji wao na kama Yanga wanamuhitaji, ni lazima waende kwao kufanya nao mazungumzo ili apate baraka za kuichezea timu yao.

Kaburu alisema kuwa baada ya kuona Yanga wakidai wamemsajili beki huyo, walipeleka malalamiko yao katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lakini hadi sasa hawajapewa jibu lolote kwavile wanaamini kuwa dirisha la usajili bado halijafungwa.

"Tutaandika rasmi barua kwa CECAFA kupinga Yanga isimtumie Yondani kwa sababu ni mchezaji wetu halali, ana mkataba na klabu yetu hivyo ni batili kuichezea timu nyingine bila idhini yetu," alisema Kaburu.

Alisema kuwa wanaamini taratibu za usajili zitafuatwa katika kufanya maamuzi sahihi juu ya utata wa usajili wa beki huyo.

"Haki ndiyo itakayomaliza mgogoro juu ya wapi Yondani anastahili kucheza," aliongeza Kaburu.

Alisema pia uongozi wa Simba unaendelea kufanya usajili na kuipa timu yao mazoezi mbalimbali ili kuhakikisha kuwa inafanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa na pia katika ligi kuu msimu ujao.

Aliongeza kwamba wao hawana wasiwasi na kikosi chao cha msimu ujao kwa sababu wachezaji wengi walio wasajiliwa ni chipukizi wenye kipaji na wenye kiu ya mafanikio.

Alisema kwamba baada ya mashindano ya Kombe la Urafiki kumalizika kesho kutwa, Simba itaendelea kubaki Zanzibar kujifua na itarejea jijini Dar es Salaam Ijumaa tayari kwa mechi yao ya kwanza ya mashindano ya Kombe la Kagame ambapo watavaana na URA ya Uganda.

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.