ZANZIBAR FOOTBALL ASSOCIATION
MEMBER OF CECAFA
ASSOCIATE MEMBER OF CAF.

|
||||
|
||||
MHESHIMIWA
WAZIRI,
WIZARA HABARI, UTAMADUNI, UTALII NA MICHEZO
ZANZIBAR.
KUH: KUSIMAMISHWA KWA KATIBU MKUU WA ZFA TAIFA
ZANZIBAR.
Tafadhali husika na mada iliopo hapo juu
aidha barua yako ya tarehe 4 Septemba
2012 yenye kumbukumbu No WHUUM/H10/1/VOL.V/33 yenye mada kama hii inahusika.
Awali ya yote naomba kutanabahisha kwamba
uamuzi wa kumsimamisha Katibu Mkuu wa ZFA Taifa umefanywa na Kamati Tendaji ya
ZFA Taifa na wala sio matakwa binafsi ya Rais wa ZFA. Mheshimiwa hayo
yanajionyesha na kuelezwa vyema katika
barua aliyotumiwa Ndugu Kassim na kunakiliwa kwako na kwengineko ya
tarehe 19 August 2012.
Mheshimiwa kwa heshima kubwa tunakuthibitishia kwamba
kwa maelekezo yako tumevirejea na
kuviangalia vyema vifungu 41 na 42 vya Katiba yetu, lakini pia tumeangalia sana
kifungu 44 cha Katiba ya ZFA kinachotowa mamlaka yasiyohojika kwa Katibu Mkuu
wa ZFA kuwajibika moja kwa kwa Rais wa
ZFA na wala sio Mheshimiwa Waziri. Lakini pia hatukuona popote palipotowa
mamlaka ya moja kwa moja kwa ngazi ya uwaziri kuteuwa Katibu Mkuu wa ZFA. Tunadhani jambo hili linafanywa kwa heshima
tu (Honorary procedure and not textual procedure), lakini bado tunaliheshimu na
tutaendelea kushirikiana katika hili. Kwani Katiba yetu haisemi wala haitaji
Rais anashauriana na nani katika uteuzi wa Katibu Mkuu ZFA.(kifungu 42)
Tumevipitia vyema vifungu 92 na 93 vya Katiba ya ZFA kama ulivyotuamuru
lakini bado tumebaini kwamba hakuna kosa
la ki-Katiba lililofanywa na Kamati Tendaji katika kumsimamisha Ndugu
Kassim kwani kifungu 94 kimetowa mamlaka
hayo kwa Kamati Tendaji ya ZFA Taifa
kumsimamaisha uongozi mjumbe yoyote.
Mheshimiwa naomba
kukumbusha kwamba kwa mujibu wa Katiba ya ZFA kifungu 31 kinaweka wazi
nani ni wajumbe wa ZFA ambapo kifungu hicho hakikumtenga Rais, Makamo, wala Katibu Mkuu wa ZFA, bali
kimesisitiza kwamba Katibu wa ZFA naye
ni mjumbe wa Kamati Tendaji na hivyo,
hatua yoyote inayopaswa kuchukuliwa chini ya kifungu 94 na yeye Katibu Mkuu wa ZFA kinamuhusu.
Mheshimiwa umeelekeza tukiangalie na kuzingatia kifungu 43 cha Katiba ambacho
umekinukuu katika barua yako, hivyo kifungu hicho tumekizingatia na tumeona
kuwa kwa tafsiri iliyo rasmi ya kifungu hicho ni kuwa kinazungumzia kipindi cha utumishi wa Katibu ZFA (tenure
of service) kwamba haiko sawa na viongozi wengine wa kuchaguliwa, kwani
Katibu anaweza akateuliwa leo na kesho
au mtondogoo akaondoshwa au akaachiwa kuendelea kwa umri wake wote.
Kifungu 43 cha Katiba ya ZFA kakitowi mwanya wowote wala kinga kwa Katibu Mkuu
kutoondoshwa, kusimamishwa, kufukuzwa au hata kuachishwa kazi.
Mheshimiwa, kwa lugha nyepesi tunaomba kusema kwamba
tumefadhaishwa na kusikitishwa sana na shutuma zilizolengwa kwetu za kuibua
dhana ya kwamba hatuithamini, hatuiamini au hatuiheshimu afisi yako. Lakini pia
kutushutumu kuwa tunaishushia hadhi afisi yako, na baya zaidi kuibuliwa hoja ya
kumuwajibisha Katibu Mkuu kwa maana ya kwamba ameadhibiwa.
Mheshimiwa kwenye hili tunalazimika kusema kwamba
hukushauriwa vyema na tunahakika kwamba washauri wako wamepitikiwa kwani Ndugu
Kassim hajawajibishwa kwa lolote, alilotakiwa ni kutowa maelezo yake kwa
maandishi kwani hio ni haki yake kwa mujibu wa Katiba ya ZFA, kama iliyoelezwa
chini ya kifungu 93 kifungu kidogo (11) cha Katiba ya ZFA. Kama mambo
hayo yameiumiza afisi yako tunaomba radhi lakini huo ndio ukweli.
Mheshimiwa, kusimamishwa kwa Ndugu Kassim haikuwa adhabu, lakini pia
kumtaka ajieleze si adhabu bali ni fursa sahihi si ya ki-Katiba tu lakini pia ni haki yake ya kibinadamu kwa mujibu wa
sharia ya nchi (natural justice and right to be heard) na tumefanya hivyo kwa
nia ya kujenga hadhi ya afisi yako na ya ZFA. Pia kuheshimu uteuzi wako na
kumpa yeye fursa ya kuleta utetezi wake juu ya shutuma anazokabiliwa nazo.
Tunadhani hatuna haja ya kuzinakili au kuzihadithia tena upya shutuma hizo
kwako kwani tumezinakili kwako kwenye
nakala ya barua aliyopewa Ndugu Kassim na tunashukuru kwa kutuhakikishia umezikuta ofisini kwako mara uliporudi safari
yako.
Mwisho, tunapenda kukiri kwamba kwa kipindi kifupi
tulichofanya nawe kazi tumebaini kwamba wewe binafsi na kwa kupitia afisi yako,
hupendi kabisa kukingia kifua maovu, hivyo basi tunaomba utowe maelekezo
yatakayomsaidia ndugu yetu Kassim kutowa maelezo yake ya maandishi
kujitetea dhidi ya shutuma anazoshutumiwa nazo ili ukweli wa jambo hili uweze
kujuilikana na haki dhidi yake kutendeka vyenginevyo bado ataendelea kuonekana
mkosaji na sisi mbele yako hatutakuwa na jengine la kusema zaidi ya kuendelea
kumshutumu kwa maovu.
Mheshimiwa hatuna nia ya kupinga amri yako, lakini
tungekusihi kwa heshima zote ukaangalia uwezekano wa kumshauri ndugu yetu
mpenzi Kassim Haji Salum kujibu hoja zinazomkali kwa mujibu wa Katiba ya
ZFA.
Mheshimiwa Waziri, tunakushukuru sana kwa
barua yako na tunapenda kukuhakikishia kuwa ZFA tumejipanga vizuri sana katika
kuondosha kadhia na migogoro yote ya ki-uongozi, ki-utendaji na ki-uendeshaji
ili ZFA iweze kusimamia maendeleo ya mchezo wa football Zanzibar.
Ahsante,
……………………………………
ALHAJJ
HAJI AMEIR
KAIMU
RAIS WA ZFA- ZANZIBAR.
NAKLA:-
1. KATIBU MKUU -HABARI ,UTALII
NA MICHEZO- ZANZIBAR
2. MWENYEKTI –BARAZAA LA TAIFA
LA MICHEZO-ZANZIBAR
3. KATIBU MTEDAJI-BARAZA LA
TAIFA LA MICHEZO-ZANZIBAR.
4. MAKAMO WA RAIS ZFA-UNGUJA
5. MAKAMO WA RAIS ZFA-PEMBA
6. KAIMU MSAIDIZI KATIBU MKUU
ZFA-PEMBA
0 comments:
Post a Comment