TFF

YAMETIBUKA UCHAGUZI TFF:- LUKAMBURA AAPA KWENDA MAHAKAMANI

Tanzania iko katika hatari ya kuingia katika mgogoro mwingine mkubwa wa soka baada ya mmoja wa waliokuwa wagombea katika nafasi ya urais wa Shirikisho la Soka (TFF), Richard Lukambura kuapa kwenda mahakamani kwa nia ya kupinga uamuzi wa kuenguliwa kwake.

Mapema mwaka huu, Lukambura alifungua kesi katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza akisimamisha uchaguzi wa TFF kwa sababu ya kuondolewa kuwania urais baada ya kamati ya uchaguzi ya TFF kueleza kwamba hana uzoefu na cheti chake kina utata.

Lukambura ameondolewa kwa sababu amekiuka katiba ya TFF ambayo katika ibara ya 12(2) (e) inazuia kupeleka masuala ya soka kwenye mahakama za kawaida za nchi.

Akizungumza kwa njia ya simu na NIPASHE jana, Lukambura alisema kwamba ameamua kwenda mahakamani kwa sababu anaona akikata rufaa kwenye Kamati ya Rufaa hatatendewa haki kutokana na wajumbe walioko kwenye kamati hiyo kuwa na dhana ya kuona kuwa daima yeye ni mkosaji tu.

Lukambura alisema kwamba anashangaa kuona ameondolewa katika mchakato huo wakati Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) liliagiza kufuta yote yaliyotokea katika zoezi hilo kabla ya kusimamishwa na kuelekeza kila kitu kianze upya.

"Hivi sasa wameweka Sh. milioni moja kukata rufaa. Kiasi hicho ni bora nisitoe na niende mahakamani kutafuta haki yangu... hapa naandaa vielelezo na nitatinga mapema wiki ijayo," alisema Lukambura.

Samuel Nyalla, ambaye alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji kwa muda wa miaka nane, naye alisema vilevile kwamba anakata rufaa kwa sababu kikatiba, anaamini kwamba yeye ana sifa zote zinazotakiwa kuwania uongozi.

"Hicho kipengele cha malengo katika fomu yangu sikukiona, nisingeweza kukiacha... nitakata rufaa na naamini haki itatendeka. Nisingeweza kuacha kujaza kipengele hicho, nadhani kuna makosa yalifanyika," alieleza Nyalla kutoka Mwanza.

Wengine ambao wameliambia gazeti hili kwamba wanakata rufaa kupinga maamuzi hayo ni mjumbe anayemaliza muda wake, Eliude Mvella na Ayoub Nyenzi, wote kutoka Iringa.

Mwisho wa kuwasilisha rufaa ni kesho saa 10:00 jioni wakati uchaguzi unatarajiwa kufanyika Oktoba 28, ukitanguliwa na uchaguzi wa Bodi ya Ligi Kuu utakaofanyika Oktoba 18 mwaka huu


source: NIPASHE

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.