Kikao cha Kamati ya Kusimamia na Kuendesha ligi (Kamati ya Masaa 72) kimekutana Jumatano katikati ya wiki kupitia taarifa na ripoti mbalimbali za michezo ya Ligi Kuu (VPL), na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) zinazoendeea kutimua vumbi katika viwanja mbalimbali nchini.
Wachezaji Ismail Nkulo, Said Juma, Idd Seleman na Edward Amos wa Polisi Dodoma wanapelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu baada ya kumzonga, kumtolea lugha ya matusi ya nguoni na kutaka kumpiga Refa katika mechi ya Ligi ya StarTimes kati ya timu yao na African Lyon iliyofanyika Januari 30, 2016.
Kitendo hicho katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma ni kinyume cha Kanuni ya 37(7) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu udhibiti wa wachezaji.
Kiongozi wa Friends Rangers, Heri Mzozo anapelekwa Kamati ya Nidhamu kwa kutoa lugha chafu kwa viongozi na waamuzi muda wote wa mchezo dhidi ya Ashanti United uliofanyika Januari 31, 2016 kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam. Vitendo vyake ni kiyume na Kanuni ya 41(2) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu udhibiti wa viongozi.
Klabu ya Geita Gold imepigwa faini ya sh. 1,000,000 (milioni moja) na onyo kali kwa kukataa kuingia kwenye chumba cha wachezaj, na badala yake kutumia chumba kingine ambacho pia walijisadia haja ndogo wakati wa mechi dhidi ya Polisi Tabora iliyofanyika Januari 31, 2016 kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Nayo Polisi Tabora imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na kitendo cha mshabiki wake kupita pembezoni ya uwanja (running track) kwa kasi wakati mechi hiyo dhidi ya Geita Gold ikiendelea.
Pia klabu ya Polisi Tabora imepewa onyo kali kutokana kipa wa timu yake kuvaa jezi ambayo haikuwa na nembo (logo) ya Mdhamini wa Ligi Daraja la Kwanza wakati wa mechi hiyo.
Geita Gold imepewa ushindi wa pointi tatu na mabao matatu baada ya JKT Oljoro kugomea mchezo kati ya timu hizo uliofanyika Februari 6, 2016 kwenye Uwanja wa Nyankumbu Girls mkoani Geita. Timu hiyo iligomea mechi hiyo dakika 70 baada ya kufungwa bao la pili. Kitendo hicho ni kinyume cha Kanuni ya 29(1) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Pia JKT Oljoro imepigwa faini ya sh. 1,000,000 (milioni moja) kutokana na kitendo hicho kwa kuzingatia Kanuni ya 29(4), wakati wachezaji wake Kapteni Shaibu Nayopa na Sunday Paul waliomvamia na kumpiga Refa wanapelekwa Kamati ya Nidhamu kwa ajili ya kuchukuliwa hatua stahiki.
Naye Kocha Msaidizi wa JKT Oljoro, Bunu Abdallah ambaye alitolewa kwenye benchi la timu yake kwa kosa la kumtolea lugha chafu Mwamuzi Msaidizi namba 1 anapelekwa Kamati ya Nidhamu kwa ajili ya hatua stahiki.
0 comments:
Post a Comment