TIMU ya netiboli ya wanawake ya JKT Mbweni inazidi kung’ara katika michuano ya Afrika Mashariki baada ya jana kushinda katika mchezo wake wa pili dhidi ya MOICT ya Kenya kwa mabao 41-37.
Katika mchezo wa juzi, maafande hao walifanya vizuri baada ya kuanza vyema michuano hiyo kwa kuifunga Polisi Uganda mabao 42-36 na hivyo kuleta matumaini ya kutwaa ubingwa.
Akizungumza baada ya kumaliza mechi hiyo, nahodha wa JKT Mbweni, Mwanaidi Hassan alisema mchezo ulikuwa ni mzuri kwao kwa vile walikuwa wakiongoza katika robo tatu ya mchezo huo.
“Tuliocheza nao leo ni wap inzani wetu kila tunapokutana katika michuano hii, lakini tunashukuru Mungu tumecheza vizuri na kuongoza robo tatu, tuna imani ya kufanya vizuri katika michuano ijayo,” alisema Mwanaidi.
Aidha, timu ya wanawake ya Mafunzo Zanzibar ilipoteza mchezo wake baada ya kupata kipigo cha Polisi ya Uganda iliyokuwa ikiongoza mabao 37-34 ikiwa na tofauti ya mabao matatu.
Mafunzo bado ina matumaini ya kusonga mbele hasa baada ya kufanya vizuri katika mchezo wake wa kwanza kwani iliishinda Ganec kwa mabao 27-25.
Wakati huo huo, timu ya wanaume ya Kazaroho ilikubali kichapo baada ya kufungwa na Polisi Zanzibar kwa mabao 56-37. Licha ya kichapo timu hiyo ina uwezekano wa kufanya vizuri baada ya kushinda mchezo wake wa kwanza dhidi ya Jiji Arusha kwa mabao 33-21.
Timu nyingine ni Mangaya ya Dar es Salaam ilipelekeshwa katika mchezo wao dhidi ya mabingwa wa Kombe la Afrika Mashariki kwa kukubali kichapo cha mabao 73-3.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA), Zainabu Mbiro alisema mchezo ni mzuri na wamefurahi kujitokeza kwa timu nyingi za wanaume, na kuongeza kuwa licha ya upinzani mkali, wanaamini baadhi yao watafanya vizuri.
CHANZO: HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment