netball

JKT MBWENI YAANZA VYEMA AFRIKA MASHARIKI

TIMU ya netiboli ya JKT Mbweni jana ilianza vizuri mashindano ya Afrika Mashariki baada ya kuifunga Polisi Uganda kwa bao 42-35 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Hadi mapumziko, JKT Mbweni walikuwa mbele kwa mabao 18- 17 na kuifanya timu hiyo kuwa katika nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi.

Katika mchezo wa wanaume, timu ya Kazaroho ya Dar es Salaam jana ilianza vizuri mashindano ya Afrika Mashariki baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 27-25 dhidi ya Ganec ya Kenya, katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa.

Mashindano hayo ambayo yanashirikisha timu mbili za wanawake za Tanzania na zingine kutoka Uganda na Kenya, yalianza juzi kwenye uwanja huo.

Timu ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Kenya iliitambia MOICT kwa mabao 48-25 katika mchezo mwingine uliofanyika kwenye uwanja huo huo wa Taifa.

Katika mchezo huo wa wanawake, Wizara ya Habari ya Kenya ilifanya kweli kwa kuibuka na ushindi katika robo zote za mchezo kwa 11-5, 20-9 na 37-17.

Katika mchezo mwingine, timu ya Kujenga Uchumi ya Zanzibar (JKU) ilishindwa kutamba mbele ya Prisons ya Uganda baada ya kuchapwa mabao 35-30.

Waganda hao wanawake walitamba katika robo zote kwa kushinda 8-6, 19-13 na 28-18 na kuibuka kidedea katika mchezo huo.

Mashindano hayo yanaendelea tena leo kwenye Uwanja huo wa Taifa huku timu nyingi zikitarajiwa kushuka dimbani baada ya jana kucheza timu sita tu ili kupisha mechi ya Ligi Kuu soka ya Tanzania Bara kati ya Simba na Coastal Union ya Tanga.

Mechi mbili za mwanzo jana ilibidi zisimame kwa muda baada ya kunyesha mvua na kufanya viwanja kuteleza na wachezaji kuanguka ovyo uwanjani. Mechi hizo ziliendelea baada ya kumalizika mvua na viwanja hivyo viwili kuondolewa maji na mifagio.

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.