KAMATI ya Rufaa na Usuluhishi ya Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) imeipa ushindi wa pointi tatu timu ya Malindi na kutengua maamuzi ya ZFA Taifa ya kurudiwa kwa mchezo kati ya timu hiyo na Miembeni.
Uamuzi huo umetokana na timu zote mbili kupinga maamuzi ya ZFA ya kurudiwa kwa mchezo baada ya timu ya Miembeni kudaiwa kumchezesha mchezaji Nassor Mohammed akiwa si mchezaji halali wa timu hiyo.
Katika matokeo ya uwanjani, miamba hiyo ilitoka kwa timu ya Miembeni kushinda bao 1-0, ambapo baadae timu ya Malindi ilikata rufaa kwa timu hiyo kumchezesha mchezaji huyo ambaye alidaiwa kutoka timu ya Arizona.
Katika barua hiyo iliyotolewa juzi na kamati hiyo imeeleza kuwa, imechukuwa maamuzi hayo baada ya timu ya Miembeni kufanya udanganyifu wa kufoji saini ya mchezaji huyo.
Kwa mujibu wa barua hiyo, kama Miembeni isingefanya udanganyifu huo kosa lote kuhusu mchezaji huyo lingeweza kuwaangukia viongozi wa ZFA Kaskazini B ambao ndio waliofanya makosa ya kumfanyia uhamisho mchezaji huyo huku wakijua kuwa sio sahihi.
“Laiti ingekuwa sio udanganyifu wa kughushi saini ya mchezaji, Miembeni ingekuwa haina kosa na badala yake kosa lingewaangukia moja kwa moja ZFA Wilaya ya Kaskazini B na hivyo kamati ingekubaliana na maamuzi ya ZFA Taifa ya kurejewa kwa mchezo,” ilieleza sehemu ya barua hiyo ambayo imetiwa saini na katibu wake Mzee Zam Ali.
Aidha, kamati hiyo mbali na kutoa maamuzi hayo, pia imemsimamisha mchezaji huyo kucheza soka hadi msimu ujao na atalazimika kufanyiwa uhamisho kutokea ZFA Wilaya ya Magharibi.
Sambamba na hilo, kamati hiyo imesema kuwa imegundua udanganyifu mwingi kufanywa na katibu wa ZFA Wilaya ya Kaskazini kwa kujaribu kuifanya haramu iwe halali, hivyo iliitaka ZFA Taifa kufuatilia suala hilo kwa uzito unaostahiki na kuchukua hatua za kinidhamu kwa katibu huyo.
CHANZO: HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment