kitaa

VURUGU MICHEZONI: WAZIRI ANUSURIKA, MJAMZITO AJERUHIWA

NAIBU Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele pamoja na mjamzito, walipata mshituko na kujeruhiwa katika vurugu zilizotokea juzi kwenye Uwanja wa Kambarage mjini hapa,(Shinyanga) baada ya kumalizika kwa mchezo wa Kundi C Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara kati ya wenyeji Stand United na Polisi ya Mara.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Evarest Mangala alisema ofisini kwake jana kuwa vurugu hizo zilitokea baada ya kumalizika kwa pambano hilo na wachezaji wa Polisi Mara kumfuata mwamuzi wa mchezo huo, Alanus Lwena kutoka Mwanza, kumuuliza sababu za kulikataa bao la kusawazisha walilofunga.

Kamanda Mangala alisema chanzo cha vurugu hizo ni baada ya wachezaji wa Polisi kumzingira mwamuzi huyo na kuanza kumhoji sababu ya kulikataa bao lao na mashabiki wa Stand United kuuvamia uwanja kwa lengo la kutaka kuwadhibiti na kuwaadhibu wachezaji waliomzingira mwamuzi.

Polisi walilazimika kuingilia kati hali hiyo kwa kutumia mabomu ya kutoa machozi ili kuwatawanya mamia ya mashabiki waliouvamia uwanja na kutaka kuyanusuru maisha ya waamuzi ambao sasa walionekana kuwa hatarini kutokana na mashabiki hao kurusha mawe na chupa za maji uwanjani baada ya kuingia ndani ya uzio wa uwanja,” alisema Kamanda Mangala.

Katika vurugu hizo, Naibu Waziri Masele, mjamzito na mwamuzi wa Daraja la Tatu mkoani hapa, Edson Lutaselwa walijeruhiwa na mpaka jana mwamuzi na mama mjamzito walikuwa wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga kwa uchunguzi na matibabu.

Katika mchezo huo, Stand United iliishinda Polisi Mara kwa bao 1-0 lililofungwa katika dakika ya 35 na kufufua upya matumaini ya timu hiyo kucheza Ligi Kuu msimu ujao baada ya kujikusanyia pointi 23 na kushika nafasi ya pili, nyuma ya ndugu zao Mwadui F.C. iliyofikisha pointi 26.

Akizungumza muda mfupi uwanjani hapo juzi, Masele ambaye pia ni Mbunge wa Shinyanga Mjini kupitia CCM, alisema vurugu hizo zimetokana na kuongezeka kwa timu za majeshi katika soka, lakini akalitupia lawama Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, kwa kuanzisha vurugu wakati pambano lilikwisha malizika.

Katika mchezo mwingine uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa Mwadui, wenyeji Mwadui F.C iliwaadhibu mabingwa wa zamani wa Tanzania, Pamba ya Mwanza kwa mabao 4-1 na kujikita kileleni mwa msimamo wa Kundi C la Ligi Daraja la Kwanza.


CHANZO: HABARI LEO

About kj

0 comments:

Powered by Blogger.