UONGOZI wa timu ya soka ya Kagera Sugar, umemtupia virago mshambuliaji wake Ahmed Shibori aliyejiunga na timu hiyo kwa mkopo akitokea Simba mwanzoni mwa msimu huu.
Hatua hiyo imekuja baada ya mchezaji huyo kushindwa kuitumikia timu hiyo tangu alipojiunga nayo kutokana na kuwa majeruhi kwa kipindi chote hicho jambo lililousukuma uongozi wa Kagera Sugar kumrudisha Simba ambao ndiyo waliokuwa wakimlipa mshahara.
Kocha msaidizi wa Kagera Sugar, Mrage Kabange alisema kuwa tayari uongozi wa timu hiyo umekwisha wasiliana na Simba na sasa wapo katika mchakato wa kutafuta mchezaji mwingine wa kuziba nafasi hiyo.
Shiboli aliyesajiliwa na Simba kwa mbwebwe nyingi akitokea timu ya KMKM ya Zanzibar, ameshindwa kuonyesha kiwango chake kilichomfanya kubakia Bara baada ya michuano ya Chalenji mwaka jana.
"Hivi sasa tupo katika mchakato wa usajili kwa ajili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ili kuimarisha safu yetu ya ushambuliaji ambayo kwenye mzunguko wa kwanza haikuonyesha makali yake kama tulivyotarajia.
"Baada ya kuondoka kwa Gaudiance Mwaikimba tuliamini kuwa Shiboli angeweza kuziba nafasi yake lakini ndiyo hivyo tena katika kipindi chote alichojiunga na sisi amekuwa nje ya uwanja," alisema Kabange.
Alisema tayari uongozi wa Kagera umeiandikia barua Simba juu ya uamuzi huo na sasa wapo katika harakati za kumsajili, Yona Ndabila ambaye hivi sasa anakipiga katika timu ya Daraja la Kwanza ya Mbeya City.
Hata hivyo, Ofisa habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema bado hawajapata barua ya Kagera Sugar juu ya suala hilo isipokuwa wana taarifa za mdomo.
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment